Share news tips with us here at Hivisasa

Wamiliki wa kumbi za kuonyesha filamu mjini Mombasa wameitaka bodi ya filamu nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria watakapokuwa wakifanya msako wa kunasa watu wanaouza filamu za ngono.

Kauli hii inakuja siku chache baada ya bodi hiyo kutangaza kuwa itaanzisha msako dhidi ya watu wanaouza filamu hizo nchini, huku ikisema kuwa hatua hiyo inapotosha maadili katika jamii hasa kwa watoto.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Rashid Omar mmoja wa wamiliki hao alidai kuwa mara nyingi maafisa wanaoendeleza misako ya aina hiyo huwa wanachukua fursa hiyo kuwanyanyasa wafanyibiashara.

“Sio kwamba tunaunga mkono filamu hizo chafu, lakini pia maafisa wanaofanya msako huwa wanakuja na kusumbua watu bila sababu. Hata kama hauna makosa utajipata umekatwa tu,” alisema Omar.

Wamiliki hao pia walisema kuwa maafisa wengi wa polisi huchukua fursa hiyo kuchukua hongo kutoka kwa baadhi ya wenye filamu hizo na hivyo kulemaza vita dhidi ya filamu za ngono nchini.

Katika kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, afisa mkuu mtendaji wa bodi ya filamu nchini Ezekiel Mutua alitangaza kwamba utafiti unaonesha kuwa usambazaji wa filamu za ngono unazidi kuongezeka nchini.

Wakati huo huo, afisa huyo alisema kuwa bodi hiyo itashirikiana na maafisa wa polisi kufanya msako ili kukomesha biashara hiyo haramu.