Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wakurugenzi wa bodi ya shirika la kupambana na utumizi wa mihadarati na vileo nchini, NACADA, sasa wanamtaka rais Uhuru Kenyatta kuivunjilia mbali bodi hiyo kutokana na wakurugezi wakuu kushindwa kuwajibikia majukumu yao.

Wakiongozwa na mkurugenzi wa NACADA Sheikh Juma Ngao, wakurugenzi hao walisema kwamba maafisa wakuu wa bodi hiyo wameshindwa kuwanasua vijana waliyojitosa katika janga hilo, na kumtaka rais Kenyetta kuchagua wakurugezi wengine walio na azma ya kufanya kazi.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Sheikh Ngao alisema kwamba zaidi ya vijana 25,000 ni waathiriwa wa dawa za kulevya aina ya heroini, na hujidunga sindano, huku asilimia 30 wakibugia mihadarati ya kunusu, hatua ambayo imechangiwa na baadhi ya maafisa wakuu kushindwa kuwakabili wahusika wakuu.

“Hatutakubali kuona baadhi ya wakurugenzi na maafisa wakuu wa shirika la Nacada wakizembea majukumu yao na kuharibu shughuli za kukabiliana na mihadarati na vileo nchini," alisema Ngao.

"Tunamtaka rais Uhuru Kenyatta aingilie kati swala hili na alivunjilie mbali shirika hili na wachaguliwe viongozi wengine watakaowakabilia walanguzi wakuu wa mihadarati,” aliongezea Ngao.

Ngao alisema kwamba idadi kubwa ya vijana waathiriwa hukwepa matibabu kutokana na vyakula wanavyopewa katika vituo vya kurekebishia tabia waraibu wa mihadarati na sehemu wanazohifadhi kuwa duni zaidi.

Alipendekeza kuidhinishwa uwanja wa Mombasa kuwa eneo maalum la kuifadhiwa watumizi wa mihadarati kwani eneo hilo ni kubwa zaidi badala ya kuhifadhiwa katika maeneo ya hospitali kuu ya ukanda wa Pwani.

“Tunapendekeza uwanja wa Mombasa County Stadium uidhinishwe kuwa maeneo rasmi ya waathiriwa wa dawa za kulevya kwa sababu vijana ni wengi waliyoathiriwa na tukiwapeleka katika vituo vilivyo katika hospitali zetu hawa vijana hawatatoshea. Vijana wako zaidi ya elfu ishirini na tano kaunti ya Mombasa pekee,” aliongeza Ngao.

Zaidi ya vijana 100 waliyojisalimisha kwa maafisa wa usalama ili kusaidiwa kujinasua katika jinamizi hilo walikwepa katika vituo hivyo na kurejea maskani kutokana na ukosefu wa mahitaji muhimu wanayopaswa kupewa waathiriwa hao.