Bodi ya shule ya upili ya Nyataro kaunti ya Kisii imesimamishwa kazi mara moja kwa kukiuka sheria za sekta ya elimu .
Hii ni baada ya bodi hiyo kuanza kutekeleza majukumu mengine bila kufuata sheria kama vile kutoa pesa kwa akaunti ya shule bila kuhusisha wahusika halisi ambao wanafaa kutia sahihi ili pesa zitumike.
Akizungumza nasi siku ya Alhamisi afisini mwake, mwenyekiti wa bodi ya elimu katika kaunti ya Kisii Henry Onderi alisema bodi hiyo imekuwa mamlakani kwa miezi miwili tu na kukiuka sheria za elimu.
Baadhi ya ukiukaji wa sheria uliojidhihirisha ni kama vile kumtenga katibu wa bodi ambaye pia ni mwalimu mkuu wa shule hiyo katika vikao vya bodi, kutoa pesa kwa akaunti na utekelezaji wa majukumu mengine mengi pasi kujumuishwa kwake.
“Bodi ya elimu katika kaunti ya Kisii imesimamisha kazi bodi ya shule ya upili ya Nyataro kwa kukiuka sheria za shule hiyo,” alisema Onderi.
“Bodi hiyo imekuwa ikifanya majukumu mengine bila kuhusisha katibu wa bodi hiyo ambaye ni mwalimu mkuu wa shule hiyo na hiyo ni kukiuka sheria na hatutakubali hayo kuendelea kamwe,” aliongeza onderi.