Wanachama wa muungano wa Cord wametaka vinara wa muungano huo kupewa ulinzi wa kutosha.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri baada ya gari la Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kudaiwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ya kushinikiza kubanduliwa kwa Tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC siku ya Jumatatu.

Licha ya Kamanda mkuu wa polisi jijini Nairobi Bwana Japheth Koome kukanusha madai hayo, wanachama hao walisema kuwa hawatachukulia swala hilo kwa mzaha.

Wakizungumza katika jengo la bunge la kitaifa, wanachama hao, wakiongozwa na Mbunge wa Nyando Bwana Fred Outa, walimtaka Inspekta mkuu wa polisi Bwana Joseph Boinet kulipa swala la ulinzi wa vinara hao kipao mbele.

"Kufuatia gari la kinara wetu wa Cord kukumbwa na mkasa huo siku ya Jumatatu, tungependa kumhimiza inspekta mkuu wa polisi kumpa kiongozi huyo usalama wa kutosha. Tuna hofu sana na maisha ya Bwana Raila Odinga,” alisema Outa.

Wanachama hao, wakiwemo Bwana Fred Outa, Dan Maanzo, James K'opiyo na Seneta wa Kakamega Bwana Bonny khalwalwe walisema kuwa kwa vile wanahofia maisha ya vigogo hao watatu wa mrengo wa upinzani, ni jukumu la Boinet kuwapa viongozi hao ulinzi wa kutosha.