Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wa Kasarani eneo la Migadini kaunti ya Mombasa wanaishi kwa hofu ya kupata maradhi baada ya bomba la maji taka kufurika huku maji hayo yakitapakaa kwenye makaazi.

Kutokana na mvua inayoendelea kunyesha eneo hilo maji hayo machafu yameanza kuingia katika nyumba zilizoko karibu huku hofu kubwa kwa wakaazi hao ikiwa ni kupata maradhi kama vile kipindupindu hasa kwa watoto.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumapili katika eneo hilo, wakaazi hao walisema kuwa wamekuwa wakiwaita maafisa wa manispaa katika kaunti lakini wanapuuza swala hilo.

“Hii shida ya bomba kufurika ni ya muda mrefu na tumekuwa tukiita manispaa wanasema watakuja lakini hatuoni lolote,” alisema Mercy mmoja wa wakaazi.

Wakaazi hao wanailaumu serikali ya kaunti kwa kupuuza jambo hilo licha ya kwamba kuna vitengo maalum vinavyohusika na maswala ya usafi katika kaunti.

Hata hivyo wanasema kuwa hawawezi kuchukua jukumu la kusafisha kutokana na uoga wa kukamwatwa na maafisa wa usafi.

Kijana mmoja kwa jina Jonathan Kilonzi anaeleza kwamba yeye na wenzake 4 walikamatwa na maafisa wa usafi na kufunguliwa mashtaka baada ya kupatikana wakifanya usafi wa mabomba ya maji taka.

“Kaunti imeshindwa kufanya kazi, lakini sisi kama wananchi tukijitolea kufanya usafi tunakamatwa, kama wameshindwa watuandike kazi sisi tuna uwezo wa kufanya hii kazi," alisema Kilonzi.

Wakaazi hao sasa wanaitaka serikali ya kaunti kuingilia swala hilo mara moja kabla madhara zaidi kutokea.

Hali hii inakuja huku wizara ya afya Mombasa ikitoa tahathari kwa wananchi kuwa waangalifu kutokana na tishio la kutokea kwa maradhi yanayosababishwa na uchafu.