Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba Timothy Bosire amejitokeza kuitaka tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kutoruhusu uhamisho wa wapiga kura kutoka maeneo bunge mengine hadi eneo bunge la Kitutu Masaba.
Akihutubia wakazi wa Manga siku ya Jumatatu, Bosire aliitaka tume hiyo kuhakikisha kuwa uhamisho wa wapiga kura kutoka eneo bunge la Kitutu chache Kaskazini hawaruhusiwi kusajiliwa katika eneo bunge la Kitutu Masaba, la sivyo aishurutishe tume hiyo kusitisha zoezi hilo.
"Sote tunahitaji zoezi la usajili wa wapiga kura lililo na uwazi na ni jambo la kushangaza kwamba baadhi ya watu wanahamishwa kutoka eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini hadi kwenye bunge hili ili kusajiliwa kama wapiga kura, na hii ni mbinu ya baadhi ya wapinzani wangu," alisema Bosire.
Bosire aliongezea kusema kuwa yuko tayari kutoa ushahidi kuhusiana na madai yake, huku akiitaka tume ya IEBC kufanya udadisi ya sajili ya wapiga kura ili kuwazuia wapiga kura walio na mazoea ya kuhama kutoka maeneo yao bila sababu.
"Ni hatia kwa watu kuhama kutoka eneo bunge lao ili kujisajili kama wapiga kura katika eneo bunge tofauti bila ya sababu mwafaka na niko tayari kuwasilisha ushahidi wangu kwa tume ya IEBC kutokana na madai hayo, na wakati umewadia kwa tume ya IEBC kuchunguza sajili ya wapiga kura," liongezea Bosire.
Bosire vilevile aliongeza kwa kusema kuwa ana mpango wa kuwasilisha mswada bungeni, mswada utakao weka matakwa makali kwa yeyote anayetaka kuhama kutoka eneo bunge lake ili kujisajili kwingine.
"Watu wamekuwa na mazoea ya kutumia vibaya uhuru wahamia sehemu zingine ili kujisajili kama wapiga kura, na nina mpango wa kuwasilisha mswada bungeni utakaokuwa na masharti makali ili mtu kuruhusiwa kujisajili katika eneo bunge tofauti," alihoji Bosire.