Mbunge wa kitutu masaba Timothy Bosire alikosa hatua ya kutotambulishwa kwa wananchi na naibu wa rais William Ruto wakati aliwatambua wabunge wengine licha ya yeye kuwepo kwenye ziara ya rais Uhuru Kenyatta kaunti ya Nyamira siku ya Jumatano.

Share news tips with us here at Hivisasa

Ruto aliwatambua viongozi wote waliokuwa kwenye mikutano mitatu ambayo walifanya kuwahutubia wananchi wa kaunti ya Nyamira, lakini hakumtambulisha Bosire hata kwa mkutano mmoja. 

Aidha, Rais Uhuru Kenyatta alimsuta na kumtuma Bosire kwa kiongozi wa chama cha Cord Raila Odinga aache siasa za fitina na kutafuta mbinu mwafaka za kupitisha maswala yake kwa serikali ama wananchi kuliko maandamano na siasa za kutenganisha wananchi. 

"Wewe Bosire, ambia kiongozi wako kuna njia nzuri na rahisi za mawasiliano, sio lazima kila mara kelele kelele, atafute njia mbadala ya kuunganisha wakenya kuliko kuwatenganisha," alisema Uhuru.

Hivi majuzi wakati rais akihutubia bunge, mbunge huyo alikataa kusimama kupeana heshima kwa wanajeshi wa Kenya ambao waliangamia nchini Somalia mbali na kumpigia filimbi pamoja na wabunge wengine wa mrengo wa Cord kama njia ya kumzuilia kuhutubia bunge hilo. 

Viongozi hao walihutubia wananchi katika mji wa Nyamira ambapo walifanya hospital ya Nyamira kuwa ya mafunzo na rufaa, mji wa Kebirigo ambapo walizindua ujenzi wa barabara ya Kebirigo-Metamaywa na hatimaye kumalizia kwa uzinduzi wa chuo cha anuai cha Ekerubo Gietai.