Baada ya utafiti wa shirika moja nchini kuonyesha kuwa Rais Uhuru Kenyatta angali na umaarufu wa asilimia 44.5 dhidi ya kiongozi wa muungano wa CORD Raila Odinga, mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba Timothy Bosire ameshtumu vikali utafiti huo.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu siku ya Jumatatu, Bosire alisema kuwa utafiti huo haudhihirishi ukweli wa mambo, huku akihoji kuwa matokeo ya utafiti huo ni kutaka kuhujumu juhudi za kinara wa CORD kuwania urais.
"Inashangaza sana kwamba utafiti unaweza fanywa na kuonyesha kuwa Rais Uhuru Kenyatta angali ana umaarufu miongoni mwa wakenya kumshinda Raila, ilhali serikali ya Jubilee imeshindwa kukabili ufisadi serikalini," alishangazwa Bosire.
Bosire aidha aliongeza kwa kulalamikia uhalali wa utafiti huo ikizingatiwa kwamba baadhi ya wanasiasa wasio wania urais walijumuishwa kwenye utafiti huo.
"Ikiwa utafiti huu ni halali inawezekanaje kwamba baadhi ya wanasiasa akiwemo naibu Rais William Ruto anaweza jumuishwa kwenye utafiti huo ilhali yeye hawanii urais," aliongezea Bosire.