Walimu wakuu wa shule za msingi na upili wanaopewa mamlaka ya kusimamia pesa za miradi mbalimbali zinazotengwa na hazina ya maendeleo ya maeneo bunge nchini wameonywa vikali dhidi ya kuvuja pesa hizo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea kwenye hafla ya kuchangisha pesa katika shule ya msingi ya Karantini, mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire alisema baadhi ya walimu wamekuwa na mazoea ya kuvuja pesa za umma, huku akirejelea kisa ambapo walimu wakuu wawili kutoka eneo walihusishwa na tuhuma za uvujaji wa pesa za miradi mbalimbali shuleni. 

"Pesa za ustawishaji wa maeneo bunge sio za kuwanufaisha watu binafsi, bali ni za kuendesha miradi muhimu shuleni, na ninaahidi ya kwamba nitakabiliana na yeyote atakayejihusisha na uvujaji wa aina hiyo kwa kuwa sitaki kuona mambo yaliyotokea kwenye shule ya msingi ya Biticha na Gachuba yakijirudia," alisema Bosire.

Mbunge huyo aidha aliongeza kusema kuwa afisi yake tayari inafuatilia miradi inayofadhiliwa na pesa za ustawishaji wa maeneo bunge, huku akionya kuwa yeyote atakayepatikana akiwaajiri wanakandarasi wanaofanya kazi duni kwa malengo ya kutengeneza pesa zaidi watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

"Nawahakikishia kuwa afisi yangu inafanya udadisi kubaini ubora wa miradi inayofadhiliwa na pesa za ustawishaji maeneo bunge CDF hasa kwenye shule za umma kwa maana sitaki kuona watu wakiajiri wanakandarasi wanaofanya kazi duni ili wajinufaishe kifedha," aliongezea Bosire. 

Kulingana na mbunge huyo wa Kitutu, shule zinazotumia pesa hizo vizuri zina uwezekano wa kufadhiliwa tena siku za mbeleni. 

"Ninazingatia shule kwa sababu mara nyingi sisi hupatiana shule za umma hundi za kufadhili miradi na shule yeyote ile ambayo itatumia pesa zake vizuri ina nafasi ya kupokezwa pesa kwa mara nyingine tena," alisisitiza Bosire.