Mbunge wa eneo la Kitutu Masaba Timothy Bosire amejitokeza kuwataka wanachama wa bodi ya tume ya mitihani nchini ambao walisimamishwa kazi kujitokeza na kuwaomba wakenya msamaha kutokana na kuwepo udanganyifu kwenye mitihani ya kitaifa mwaka jana.
Kwenye mahojiano ya kipekee siku ya Jumatatu, Bosire alisema kuwa yafaa maafisa wa tume hiyo wajitokeze kuwaomba wakenya msamaha kutokana na kuwepo udanganyifu kwenye mitihani ya kitaifa mwaka jana.
"Kwa kweli maafisa wa tume ya KNEC wanastahili kujitokeza hadharani na kuwaomba wakenya msamaha kwa sababu ya kuwepo udanganyifu wa mitihani mwaka jana, na hata baada ya vyombo vya habari kutangaza wazi kuwepo kwa udanganyifu huo maafisa hao walipuuza," alisema Bosire.
Bosire aidha aliongeza kwa kuitaka serikali ya kitaifa kuwachukulia hatua kali maafisa wa tume hiyo iwapo hawatojitokeza kuwaomba wakenya msamaha.
"Ikiwa wahusika wakuu wa visa vya udanganyifu wa mitihani hawatojitokeza kuwaomba wananchi msamaha, basi yafaa washikwe nakuwasilishwa mahakamani ili kuwajibikia vitendo vyao," aliongezea Bosire.