Mbunge wa Kitutu Masaba Timothy Bosire ametangaza mpango wa kujengwa maktaba ya kisasa kwenye wadi ya Rigoma ili kusaidia watu kupata mafunzo katika eneo hilo. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Bosire alidokeza hayo alipoitembelea shule ya upili ya Nyabiosi mapema Alhamisi pale aliponukuliwa akisema kuwa maktaba hiyo itasaidia pakubwa kupevusha akili za vijana wa eneo hilo ili waimarishe uchumi wa eneo hilo kwa kubuni mbinu zitakazosaidia kuinua hadhi ya eneo hilo.

"Maktaba hiyo itakuwa na umuhimu mkubwa kwa kuwa itasaidia pakubwa kuinua viwango vya elimu miongoni mwa wenyeji wanaosomea vitengo mbalimbali vya elimu, na nina furaha kwamba baadhi ya marafiki wangu wanaoishi marekani wamekubali kutupa msaada," alisema Bosire. 

Mbunge huyo wa Kitutu aliongeza kwa kusema kuwa mradi huo ulibuniwa na wasomi wa eneo bunge lake, huku akiongeza kusema kuwa ujenzi wa maktaba hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka wa 2016,  na yeyote atakayetaka huduma za maktaba hiyo hatolipishwa lolote kwa kuwa huduma zitapeanwa bila malipo.

"Sidhani kuwa mahala pa kujengwa maktaba hiyo pataleta shida kwa kuwa tayari nimesha washauri wasomi mbalimbali na ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka wa 2016, na yeyote atakaye hitaji huduma za maktaba atazipata bila malipo," aliongezea Bosire.