Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Bunge la Kaunti ya Mombasa limepitisha hoja inayompa gavana wa kaunti hiyo mamlaka ya kuzipa majina barabara za kaunti.

Mwakilishi mteule katika bunge hilo Mohamed Hatimi aliwasilisha hoja hiyo bungeni siku ya Jumatano inayosema kuwa gavana atakuwa na mamlaka ya kuzipa barabara hizo majina ya watu ambao wameleta mabadiliko katika maendeleo ya taifa.

Mbali na barabara, gavana pia atakuwa na mamlaka ya kuyapa majengo ya mjini humo majina ya watu mashuhuri.

Haya yanajiri baada ya kiongozi wa Cord Raila Odinga pamoja na Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuzindua rasmi barabara ya Fidel Odinga mjini Mombasa.

Hatua hiyo iliibua hisia kali kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari humu nchini, huku baadhi ya Wakenya wakipinga vikali barabara hiyo ya Nyali kupewa jina hilo.

Wengi waliitaja hatua hiyo kama isiyo na umuhimu kwa Wakenya huku Gavana Joho akitetea hatua hiyo na kusema kwamba ilikuwa ni zawadi kwa kiongozi huyo wa Cord.

Uzinduzi wa barabara hiyo uliwafanya wengi kujiuliza iwapo marehemu Fidel aliwahi kufanya lolote kwa maendeleo ya taifa kiasi cha kutengewa barabara.