Bunge la kaunti ya Nyamira limelalamikia pakubwa utendakazi wa kamati ya huduma za umma huku likitawataka wanachama wa kamati hiyo kubanduliwa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakijadili suala la wanachama wa kamati hiyo hasa mwenyekiti wa James Mating'a kukosa kuwa bungeni ili kutoa mstakabali kuhusiana na masuala yanayoambatana na kamati hiyo wawakilishi wadi mbalimbali walitaka wanachama hao wachukuliwe hatua. 

Akitoa mchango wake, mwakilishi wa wadi ya Gesima Atuti Nyameino aliliambia bunge kuwa kamati ya huduma za umma haichukulii majukumu yake kwa uzito.

"Ukweli ni kwamba wanachama wa kamati ya huduma za umma wanachukulia majukumu yao humu bungeni kimzaha tu na nadhani wakati umefika kwa wanachama hao kuadhibiwa," alisema Nyameino. 

Kwa upande wake kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti hiyo Laban Masira alisema kuwa yafaa naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Robert Ongwano achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kutoka bungeni wakati bunge hilo lilipotaka kujua msimamo wake kuhusiana na kukwama kwa ujenzi wa chuo cha kiufundi cha Bigege. 

"Spika ni jambo la kushangaza kwamba naibu mwenyekiti wa kamati ya huduma za umma kwenye bunge hili anaweza kusimama na kuondoka bungeni wakati tunapojadili masuala yanayohusiana na kamati yake na kwa sababu hiyo anastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu," alisema Masira. 

Hata hivyo naibu spika wa bunge hilo Andrew Magang'i alimwagiza kiranja wa bunge hilo Peter Maroro kuwachunguza wanachama wa kamati hiyo ili kuona iwapo kuna haja yakubandua baadhi yao.

"Ni agizo langu kwa kiranja wa bunge hili Peter Maroro kuhakikisha kwamba anachunguza vyema wanachama wa kamati hiyo ili kuona iwapo kuna haja ya kuwabandua baadhi yao na sharti ripoti hiyo iwasilishwe hapa bungeni jumanne wiki ijayo," alisema Magang'i.