Bunge la kaunti ya Mombasa. [Picha-Standard.]

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Bunge la kaunti ya Mombasa linatarajia kurejelea vikao vyake mapema mwezi huu baada ya kuwa na likizo ndefu.

Baadhi ya mswada ambao unatarajiwa kujadiliwa ni ule unaopendekezwa na mwakilishi wadi mteule Fatmah Swaleh ambaye anataka kupigwa marufuku kwa uuzaji wa Miraa na ‘Muguka’  Mombasa.

Mwakilishi  wadi mteule Fatmah Swaleh alisema kuwa anatayarisha mswada huo ambao ataupeleka katika bunge la kaunti ya Mombasa ili ujadiliwe.

Kwa upande wake naibu spika wa bunge hilo Fadhili Mwalimu alisema kuwa kuna miswada mingi ambayo inatarajiwa kujadiliwa ambayo imependekezwa na umma huku akiongeza kuwa wanatarajia kamati ya biashara ya bunge hilo kuwapa mwelekeo.

Mwalimu alisema kuwa wamepokea malalamishi mengi kutoka kwa umma kuhusiana na ugonjwa wa Chikungunya  ambao anasema kuwa bunge linatarajia kukuja na suluhu la kuhakikisha kuwa ugonjwa huo unaangamizwa kabisa. 

“Baadhi ya mapendekezo ambayo tumepokea kutoka kwa wakilishi wadi na umma ni kuwa serikali ya kaunti kuja na suluhu la kudumu la kuhakikisha kuwa ugonjwa wa chikungunya unamalizwa kabisa na kuzuia kuzuka tena,’’ alisema Mwalimu.

Mwalimu pia alisisitiza kuwa kuna haja ya kumaliza mkusanyiko wa takataka mjini Mombasa na kulipa swala la elimu kipaumbele.