Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amesema kuwa atafanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika bunge la wawakilishi wa wadi katika gatuzi la Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana Joho amethibitisha haya akihutubia kongamano katika ukumbi wa Swahili Culture jijini Mombasa siku ya Alhamisi 8 .

‟Wawakilishi wa wodi wa kisisiasa katika bunge letu la kaunti waweke kwamba lugha inayotakikana zaidi katika michango yao na kutunga sheria kwao iwe Kiswahili,” alisema gavana huyo.

Huenda kutangazwa kwa Kiswahili kama lugha kuu ya mawasiliano katika bunge la Mombasa kukaongeza na kuboresha mawasiliano baina ya wawakilishi wa wadi na kushuhudia visa vichache vya malumbano na sintofahamu ambavyo vimelikumba bunge hilo katika siku za hivi karibuni.

Joho pia amewasihi wanafunzi kutoka kanda ya Pwani kutia bidii katika somo la Kiswahili ili wawe kielelezo bora kwa wanafunzi wengine nchini.

‟Wanafunzi wa Pwani watie bidiii katika lugha fasihi ya Kiswahili ili wawe kielelezo bora kwa wanafunzi wengine nchini, ” aliongeza.

Kwa muda wanafunzi kutoka bara ya Kenya wamekuwa wakifanya vizuri zaidi katika somo la Kiswahili mitihani ya kitaifa licha ya kuwa Pwani ya Kenya inatumia sana lugha hii kuliko sehemu yeyote ile katika nchi.

Aidha gavana Joho pia ametaja lugha ya Kiswahili kuwa ala ya kuwashikanisha wakenya na kuvunja ngome ya ukabila inayoendelea kukita mizizi nchini.