Kuna uwezekano kuwa wanafunzi wa chuo kikuu cha ufundi cha Mombasa wakapata adhabu, huku bunge la kaunti ya Mombasa likijadili suala hilo na kupendekeza kuadhibiwa kwa wanafunzi waliohusika katika machafuko ya siku ya Jumatatu.
Mjadala huo unalenga kubuni njia za kuwatia mbaroni wanafunzi ambao hujihusisha kwenye maandamano na kuchukua nafasi yao vibaya kwa kuharibu mali ya umma, na iwapo utapitishwa, wanafunzi wa chuo hicho watakuwa wa kwanza kuathirika na mswada huo.
Mswada huo ambao ulipelekwa kwenye bunge la kaunti na mwakilishi wa wadi ya Portreitz Mwalim Fadhili uliweza kuratibishwa kwenye orodha ya mijadala, na ulijadiliwa kwenye bunge hilo kwa awamu ya kwanza siku ya Jumatano.
Mswada huo iwapo utapitishwa kuwa sheria huenda ukawaathiri wanafunzi wa chuo husika cha Mombasa kugharimia malori mawili amabyo yalichomwa kwenye pandashuka hizo za maandamano ya wanafunzi mapema wiki hii.
Viongozi wa siasa akiwemo Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho pamoja na mbunge wa eneo la Mvita Abdulswamad Shariff Nassir wamekemea kitendo hicho, na kutaka idara ya polisi kufanya uchunguzi na kuwaadhibu waliohusika na kuharibu mali ya wenyewe.
Hata hivyo, viongozi wa jumuia ya wanafunzi kutoka chuo hicho tayari wamejitokeza na kukana madai kuwa wanafunzi walihusika katika kuteketezwa kwa malori ya serikali ya kaunti ya Mombasa.