Bunge la Kaunti ya Nyamira limelazimika kuhairisha vikao vyake kwa muda wa kipindi cha wiki mbili kwa ukosefu wa fedha za kuliwezesha kuendelea na vikao vyake sawa na shughuli za kawaida katika Bunge hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na Spika wa Bunge hilo Joash Nyamoko, iliwalazimu Wawakilishi wa Bunge hilo ambao walirejelea vikao vyao siku ya Jumanne kutoka likizoni kupitisha mswada huo wa kuhairisha vikao hivyo kwa ukosefu wa pesa zao za marupurupu kwa kamati mbali mabli na pia za kulipa madeni.

Spika Nyamoko alikuwa akiongea kwenye Bunge hilo baada ya kuhairisha vikao kwa muda wa wiki mbili.

Hali hii imepelekea shughuli za kawaida kukwama ikizingatiwa kwamba ujenzi wa makao ya Bunge hilo haujakamilika.

Wawakilishi wa Wadi katika Bunge hilo kwa sasa wanakosa mahala pa kufanyia vikao vyao pamoja na afisi za wafanyakazi.

Vile vile mwanakandarasi amelazimika kusitisha ujenzi wa Bunge hilo kwa sababu ya kutolipwa kwa kipindi kirefu.

Spika Nyamoko amelaumu masaibu yao kutokana na kiwango cha chini cha walichotengewa na mamlaka ya mpito sawa na tume ya ugawi wa mapato.

Spika huyo aliongeza kwamba itawabidi wafike mbele ya tume hizo mbili kuwasilisha malalamishi yao.

Ikumbukwe kwamba sio Kaunti ya Nyamira tu imeathirika, bali Kaunti ya Kwale pia ililazimika kuendeleza vikao bila maji ya kunywa.