Hatimaye bunge la kaunti ya Nyamira limemwidhinisha rasmi aliyekuwa mkurugenzi wa wizara ya kilimo mifugo na uvuvi kwenye serikali ya kaunti hiyo kuhudumu rasmi kwenye wadhifa wa katibu wa wizara hiyo.
Wakijadili hoja ya kuidhinishwa kwake bungeni siku ya Jumanne, wabunge wa bunge hilo walisema kwamba mkurugenzi huyo Edward Ondigi amehitimu kuhudumu kwenye wadhifa huo.
Akichangia kwenye hoja hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati ya kilimo kwenye bunge la kaunti hiyo Boniface Ombori, hoja iliyowasilishwa baada ya kamati hiyo kumchuja afisa huyo, mwakilishi wa eneo la uwakilishi wadi ya Itibo Samuel Nyanchama alisema kuwa afisa huyo amehitimu kuhudumu kwenye wadhifa huo kwa maana ana tajriba ya hali ya juu kwenye masuala ya kilimo.
"Kwangu mimi naona kwamba huu ni wakati mwafaka kwa bunge hili kumwidhinisha rasmi Ondigi kama katibu wa wizara ya kilimo, mifugo na samaki kwa maana ana uzoefu wa masuala ya kilimo kwa muda mrefu," alisema Nyanchama.
Kwa upande wake mwakilishi wa eneo la Gesima Ken Nyameino, afisa huyo anastahili kuhudumu kwenye wadhifa huo kwa miaka mitatu sasa amekuwa akihudumu kama mkurugenzi wa wizara hiyo.
"Ondigi ni afisa shupavu na anayeelewa kazi yake vyema zaidi, na naona kwa huu muda wa miaka mitatu ambao amekuwa akiutumia kuifanyia hii serikali kazi kama mkurugenzi wa wizara ya kilimo unatosha kumuidhinisha kama katibu wa wizara hiyo," alihoji Nyameino.
Ondigi ana shahada ya uzamili kwenye masuala ya uratibu na usimamizi wa miradi kutoka chuo kikuu cha Nairobi na shahada ya uzalishaji wa mifugo almaarufu 'Animal production' kutoka chuo kikuu cha Egerton.