Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la kaunti ya Nyamira limepitisha mswada wa kuagiza kituo cha mafuta ya magari kilichojengwa eneo la Konate, wadi ya Bonyamatuta kiondolewe mara moja.

Mswada huo ulipitishwa siku ya Jumatano katika bunge la kaunti ya Nyamira baada ya mswada kufikishwa kwa bunge hilo na mwakilishi wa wadi ya Bonyamatuta, Robinson Mocheche kwa kudai kuwa kituo hicho kilijengwa katika chemichemi ya maji ambayo watu wa eneo hilo hutumia.

“Kituo hicho cha mafuta kilijengwa kwa kukiuka sheria za mazingira nchini na watu wa eneo hilo huyatumia maji hayo," alisema Mocheche.

Kituo hicho kimejengwa mita 50 kutoka mahala watu wanapochota maji huku serikali ya kaunti hiyo kupitia wizara ya mazingira, kusema haitakubali kuendelea kwa kituo hicho maana watu watakuwa wameathirika pakubwa.

Wakati mswada huo ulikuwa unapitishwa mwakilishi wa wadi ya Itibo, Kaunti ya Nyamira Samuel Nyachama alionekana kuupinga mswada huo kwa kusema kesi ya kituo hicho kingali kwa mahakama na kusema wawakilishi wangesubiri uamuzi wa mahakama kabla ya kuupitisha mswada huo.

Juhudi zake ziligonga mwamba kufuatia idadi kubwa ya wawakilishi kuupitisha mswada huo.

Hii si mara ya kwanza ujenzi wa kituo hicho cha magari kupingwa na wakaazi pamoja na wawakilishi wa wadi mbalimbali katika kaunti ya Nyamira.

Kwa sasa kituo hicho kitaondolewa ili mwananchi wa kawaida apate haki kwa kupata maji safi.