Mwakilishi wa eneo wadi la Manga Peter Maroro amemtaka kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Laban Masira kuwaelezea bayana sababu ya kutofahamishwa kuhusiana na ziara ya Rais Kenyatta kwenye kaunti hiyo.
Akitoa kauli yake bungeni siku ya Alhamisi, Omanga alimtaka Masira kuelezea bunge hilo sababu ya wawakilishi wadi kutofahamishwa kuhusu ziara ya kiongozi wa taifa.
"Ningetaka kiongozi wa walio wengi kwenye bunge hili kutueleza bayana sababu iliyosababisha wawakilishi wadi kutofahamishwa kuhusiana na ziara ya Rais Uhuru Kenyatta katika kaunti hii," aliuliza Maroro.
Maroro aidha alilalamikia pakubwa miradi ya maendeleo iliyozinduliwa na Rais Kenyatta katika kaunti ya Nyamira ikizingatiwa na ile iliyozinduliwa kule Kisii.
"Kuna jambo ambalo tunastahili kujua kama bunge la kaunti hii, iwapo kweli kaunti hii ni kaunti ndogo ya serikali ya Kisii au ni serikali ya kaunti inayojisimamia kivyake kwa kuwa idadi ya miradi ya maendeleo iliyozinduliwa kule Kisii na Rais Uhuru inazidi ya huku Nyamira," aliongezea Maroro.
Hata hivyo, kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kaunti hiyo aliahidi kutoa ripoti kamili kuhusiana na ziara ya Rais Uhuru Kenyatta Jumanne wiki ijayo.
"Analolalamikia mheshimiwa Maroro lina msingi na ninaomba mniruhusu kuwasilisha ripoti kamili kuhusiana na ziara ya Rais Uhuru Kenyatta hapa Nyamira Jumanne wiki ijayo," alisema Masira.