Spika wa Seneti Ekwe Ethuro katika hafla ya awali. Picha/ nation.co.ke
Spika Ekwe Ethuro amesema Bunge la Seneti kamwe haliwezi kuvunjiliwa mbali kwa kuwa ndilo msingi thabiti wa maendeleo na demokrasia humu nchini.Akizungumza siku ya Jumanne katika kongamano la kiuongozi linaloendelea Mjini Mombasa, Ethuro alisema kwamba licha ya wabunge kushinikiza kuvunjiliwa mbali kwa bunge la Seneti, bunge hilo limepigania uiano katika taifa hili.Ethuro alionya kwamba iwapo Seneti litavunjiliwa mbali, basi huenda vurugu za baada ya kura za mwaka 2007/2008 zikashuhudiwa tena katika uchaguzi wa Agosti.Spika huyo alisema kwamba taifa hili linahitaji vitengo kama bunge la Seneti na idara thabiti ya Mahakama ili kulinda demokrasia na umoja wa taifa.Aidha, alisema kwamba japo Bunge la Seneti limekuwa likikashifiwa limetekeleza jukumu kubwa mno la kuhakikisha kwamba wabunge hawapitishi sheria zinazowakandamiza wakenya.Hapo awali, Bunge la Kitaifa lilishinikiza kuvunjiliwa mbali kwa Seneti kutokana na gharama kubwa kwa mlipa ushuru.Vile vile, Ethuro amewataka vijana kuwa katika mstari wa mbele katika kupigania nafasi mbalimbali za ajira kwa lengo la kuubadili uongozi wa taifa.Ethuro alisema kwamba vijana wa miaka 35 kurudi nchini wako na nafasi nzuri mno katika kuchukua uongozi wa taifa hili na kamwe hawafai kusalia nyuma na kuwaacha viongozi wazee kuendelea kuongoza.“Inasikitisha mno kuwaona vijana wakiendelea kushabikia viongozi ambao wamekuwa mamlakani kwa muda mrefu badala ya hao kujipigia debe wenyewe kwa wenyewe ili kunyakua nafasi mbalimbali za uongozi,” alisema Ethuro.