Bunge la kaunti ya Nyamira limefutilia mbali ripoti iliyowasilishwa kwao na kamati ya uchunguzi wa utumizi wa pesa za serikali ya kaunti hiyo.
Kulingana na idadi kubwa ya wawakilishi wa bunge hilo walidai wanakamati waliokuwa wanachunguza miradi mbalimbali katika wizara tofauti walihongwa, na kusema hakukuwa na uwazi katika ripoti hiyo.
Akizungumza siku ya Jumatano katika bunge hilo, mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchunguzi wa pesa za serikali katika kauti hiyo ya Nyamira Ezra Mochiemo alidai baadhi ya wizara zilihusika na ufisadi, na kutaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya mawaziri husika.
Baadhi ya wizara ambazo zilidaiwa kuwa na ufisadi ni wizara ya barabarara na uchukuzi, ile ya maji, na ile ya vijana.
“Mawaziri wa wizara zile ambazo zilihusika na ufisadi wanastahili kuchukuliwa hatua ili uwazi kuonekana kwa wakazi wa kaunti hii kwani pesa ni za wakazi,” alisema Mochiemo.
Kamati hiyo ilitembelea miradi ya maendeleo ambayo ilifanywa na wizara hizo katika wadi mbalimbali na kuandika ripoti ambayo haikukubaliwa na wawwakilishi wadi.