Kufuatia uvamizi wa familia moja kule Nyamusi na kuwateketeza wanafamilia moja, sasa bunge la kaunti ya Nyamira limeitaka serikali ya kaunti hiyo kugharamia mazishi ya waliouawa na pia kuwalipa pesa za hospitali kwa majeruhi. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akichangia kwenye hoja hiyo bungeni siku ya Jumanne, mwakilishi maalum William Atati alisema kuwa yafaa serikali ya kaunti hiyo igharamie mazishi ya waliouawa na pia kulipa pesa za matibabu kwa watoto wa familia hiyo wanaoendelea kupokea matibabu kwenye hospitali kuu ya Kisii.

"Kwa kweli hili ni pigo kubwa sio tu kwa familia iliyoathirika bali pia kwa serikali ya kaunti hii, na ndio maana naona ni bora iwapo serikali ya kaunti ingegharamia mazishi ya waliouawa na majambazi kule Nyamusi na hata pia kuwalipia pesa za hospitali wale watoto walionusurika," alisema Atati. 

Kwa upande wake mwakilishi wa eneo wodi ya Itibo Samuel Nyanchama, alisisitiza kwamba yafaa suala la usalama wa wananchi lishughulikiwe kwa haraka.

"Tuna jukumu kama bunge kuwahakikishia wapiga kura usalama wao na kwa kweli sharti tuweke mikakati ya kuhakikisha kuwa hilo linatekelezwa," alisema Nyanchama. 

Baada ya asilimia 70 ya wawakilishi wadi katika bunge hilo kuunga mkono suala la serikali ya kaunti kugharamia mazishi ya tukio hilo naibu spika alisema kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha kuwa hilo limetekelezwa.

"Kwa kweli kuna hitaji la serikali ya kaunti hii kuchukua jukumu lakugharamia hafla ya mazishi ya wale waliouawa na hata pia pesa za matibabu kwa wanao ili kuonyesha mshikamano na familia hiyo hasa kwenye wakati huu wa huzuni," alisema Magang'i.