Huenda wakazi wa kaunti ya Nyamira hasa wanafunzi walio na changamoto za kujiunga na kidato cha kwanza na hata vyuo vikuu kutokana na ukosefu wa karo wakapata afueni iwapo bunge la kaunti hiyo litaidhinisha mswada wa kupokeza wanafunzi husika msaada wa kifedha.
Akitoa mchango wake bungeni kuunga mkono hoja hiyo siku ya Jumatano, mwenyekiti wa kamati ya elimu bungeni Samuel Nyanchama alisema asilimia hamsini ya wanafunzi werevu wanaotoka katika familia maskini hukosa kuhudhuria shule kutokana na ukosefu wa karo, hali anayosema inaathiri pakubwa ukuaji wa kaunti.
"Asilimia hamsini ya wanafunzi werevu wanaotoka kwenye familia maskini hukosa kuhudhuria shule kwa sababu ya ukosefu wa karo, na ingekuwa bora kwa bunge hili kuidhinisha mswada utakaowasaidia wanafunzi hao kupata msaada wa kifedha kwa sababu hali hii ya wanafunzi kuacha kusoma inachangia pakubwa kurudisha taifa hili nyuma," alisema Nyanchama.
Kwa upande wake kiongozi wa walio wengi kwenye bunge hilo Laban Masira, sharti bunge hilo lishughulikie suala hilo kwa haraka kwa minajili ya kuokoa vizazi vya kesho kutoka kwenye umaskini.
"Ni wajibu wetu sisi kama wawakilishi wadi kuhakikisha kwamba tunaidhinisha mswada huu iwapo kwa kweli tunataka kuepusha vizazi vya kesho kutokana na umaskini," alihoji Masira.