Bunge la Kitaifa limehimizwa kuunga mkono mswada wa kutaka serikali kutenga pesa za kuwalipa marupurupu waliokuwa madiwani kote nchini kama wafanyikazi wengine wa serikali jinsi bunge la seneti lilikubaliana na kupitisha.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi nyingi ya waliokuwa madiwani wanaishi katika hali ya umaskini kwani hawakulipwa marupurupu yao.

Wakizungumza siku ya Jumapili mjini Kisii, zaidi ya waliokuwa madiwani 300 wakiongozwa na mwenyekiti wao nchini Tom Mboya walisema itakuwa jambo la kufurahisha ikiwa bunge la kitaifa litapitisha mswada huo ili serikali kuwatengea pesa zao kama wafanyikazi wa serikali.

“Mshahara ambao madiwani wa zamani walikuwa wanakabidhiwa si mshahara wa mfanyikazi wa serikali maana ulikuwa duni,” alisema Mboya.

“Wengi wao sasa hivi wanaishi katika hali ya umaskini, tunaomba bunge la kitaifa kuitikia na kupitisha mswada jinsi seneti ilipitisha ili tulipwe marupurupu yetu kama wafanyikazi wengine wa serikali,” aliongezea Mboya.

Aidha, katibu wa waliokuwa madiwani katika kaunti ya kisii David Siro aliomba Rais Kenyatta kuitikia jambo hilo na kuahidi kumuunga mkono katika uchaguzi ujao ikiwa atashirikiana nao kwa kuunga mkono ombi hilo .

Photo: Wabunge wakiwa katika vikao hapo awali. Wabunge hao wameombwa kuunga mkono mswada wa kutaka serikali kutenga pesa za kuwalipa marupurupu waliokuwa madiwani kote nchini. Maktaba