Bunge la Kaunti ya Nyamira limepitisha mswada wa kuwanunulia wanawake wanoishi na ulemavu vitanda katika hosptali za serikali ili wawe katika hali nzuri wanapojifungua.
Hii ni baada kubainika kuwa wanawake hao husumbuka wanapojifungua kufuatia ukosefu wa vitanda vya walemavu katika hospitali za kaunti hiyo.
Mswada huo ulifikishwa bungeni siku ya Jumanne na mwakilishi wa walemavu katika kaunti ya Nyamira Richard Bosire ambaye alisema wanawake wanaoishi na ulemavu hupitia changamoto nyingi wanapojifungua kwani hushindwa kutumia vitanda vya kawaida ambavyo viko katika hospitali za kaunti hiyo.
Mswada huo ulipitiswa kupitia idadi kubwa ya wawakilishi wa bunge hilo waliomwomba Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kuutia sahihi mswada huo haraka ili uwe sheria.
“Wanawake walemavu wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu katika kaunti hii ya Nyamira ndiposa nikafikisha mswada huu katika bunge hili. Ninawashukuru wawakilishi wenzangu kwa ushirikiano walioonyesha kwa kupitisha mswada huu ili vitanda vya walemavu viwe katika hospitali za serikali hapa Namira,” alisema Bosire.
Aliongezea “Tunahitaji wanawake wanaoishi na ulemavu wanapojifunguwa wawe katika hali nzuri kama watu wengine ili maslahi yao yaweze kuafikiwa kulingana na katiba ya Kenya katika serikali za ugatuzi.”