Bunge la kaunti ya Nyamira limemwagiza mwenyekiti wa kamati ya usimamizi wa umma kwenye bunge hilo James Mating'a kuweka bayana idadi ya watu walemavu wanaofanya kazi katika kaunti hiyo. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakichangia kwenye hoja hiyo bungeni, wawakilishi wadi walimtaka Mating'a kuleta ripoti bungeni itakayoweka wazi idadi ya watu walemavu na kiwango cha ulemavu cha watu hao wanaofanya kazi kwenye kaunti hiyo. 

Mwakilishi mteule Lucy Onsusu alimtaka Matinga kuweka wazi maeneo wadi wafanyakazi hao hao wanakotoka ili bunge la kaunti hiyo libaini iwapo kuna usawa katika shughuli ya kuajiri walemavu. 

"Mimi naona kama mwenyekiti wa kamati ya usimamizi wa umma amelala kazini kwa kuwa hatujui idadi ya watu walemavu wanaofanya kazi katika kaunti hii, na ndio maana sharti ahakikishe kwamba tumejua maeneo wadi wanakotoka wafanyakazi hao kwa kuwa tunataka kubaini iwapo kuna usawa kwenye shughuli ya uajiri," alisema Onsusu. 

Kwa upande wake mwakilishi wa wadi ya Itibo Samuel Nyanchama alimtaka Matinga kueleza bunge hilo aina ya mchango wafanyikazi hao walemavu wanao utoa kwa serikali. 

"Tungependa kujua ni mchango wa aina gani wafanyakazi walemavu wanaoutoa kwenye serikali ya kaunti ili kubaini iwapo kuna umuhimu wa kuajiri wengine zaidi," alisema Nyanchama. 

Hata hivyo, naibu spika Andrew Magang'i alimwagiza mwenyekiti wa kamati hiyo kuwasilisha bungeni orodha ya wafanyakazi walemavu wanaofanya kazi katika kaunti hiyo Jumanne wiki ijayo.