Wanawake katika kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani wametakiwa kuwalinda vyema watoto wao dhidi ya dhulma za kijinsia na ubakaji uliokithiri katika eneo hilo.
Kulingana na mwenyekiti wa maswala ya watoto na jinsia ambaye pia ni Mwakilishi maalum katika bunge la Kaunti ya Mombasa Bi Serah Nyamvullah, asilimia kubwa ya visa vya ubakaji hutendewa watoto wadogo na akina mama wasiojiweza, hali ambayo inastahili kudhibitiwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Nyamvullah alisema kwamba serikali kuu imekumbwa na changamoto katika kulinda haki za mtoto na mwanamke, hali iliyopelekea ongezeko la dhulma za kijinsia katika jamii.
Amesema kwamba ongezeko la visa vya ubakaji, dhuluma nyinginezo za kjinsia na ukandamizaji wanaoshuhudia wanawake katika eneo hilo ni ishara kamili kuwa taifa hili lingali nyuma katika kumwangazia mwanamke na mtoto.
Aidha, imeitaka serikali kuu na ile ya kaunti ya Mombasa kutumia sheria zilizopo katika kuwaadhibu wale wanaomnyanyasa mwamake na mtoto katika eneo zima la Pwani, huku akiwashinikiza akina mama kusimama kidete na kupigania haki zao kikamilifu.
"Ni lazima kwa serikali kuu na zile za kaunti kujitokeza na kutumia sheria zilizopo kikamilifu na kumlinda mtoto na mwanamke dhidi ya dhuluma za kijinsia na ubakaji ili taifa hili kuwa huru kwa mwamanke na mtoto wa kike," alisema Nyamvullah.
Hata hivyo, ameahidi kushirikiana na viongozi wenza katika kuendeleza kampeni kuhusiana na jinsi jamii ya Mombasa na eneo la Pwani kwa jumla litakavyokabiliana barabara na dhuluma zinazomkumba mwanamke na mtoto.