Chifu wa Kata ya Pundo katika eneo la Maseno, Dominic Okumu amepiga marufuku kuandaliwa kwa burudani la muziki nyakati za usiku baada ya hafla ya mazishi.
Okumu ameonya kuwa hali hiyo imewapotosha vijana wengi huku wengi wa vijana wakiacha masomo.
Okumu alisema kuwa eneo hilo ndilo linaloongoza kwa idadi ya visa vya vijana kuacha shule na kujifunza kunywa pombe wakiwa na umri mdogo katika kaunti hiyo.
“Hatutaki kuwa na kizazi potovu siku za usoni kwa sababu ya raha nyingi. Iwapo mtu yeyote katika eneo hili atapatwa na shida ya msiba tafadhali naomba ulinde wageni wako kwa njia nyinginezo tulivu bila kelele za muziki na pombe,” alisema Okumu.
Okumu alikuwa akizungumza katika hafla ya mazishi iliyokuwa katika kijiji hicho cha Aloka mnamo siku ya Jumanne ambapo alisema kuwa amechoshwa na kesi za watu kupigana baada ya hafla za mazishi.
“Tutakuwa tukifanya msako na kuwatia baroni watu ambao watakiuka maagizo haya. Pia tutawashika watu ambao wana tabia ya kuvuruga amani wanapolewa,” alisema Okumu.
Eneo hilo limekuwa na visa vya watu kupigana baada ya matanga vilevile visa vya wanafunzi kuacha shule zimekuwa zikiongezeka.