Mwanamme anayedaiwa kumtusi mke wake kuwa ni kahaba amefikishwa mbele ya mahakama moja ya Nakuru Jumanne kujibu shtaka hilo.
Mshtakiwa huyo anayefahamika kama Samwel Kamau anadaiwa kutekeleza kosa hilo tarehe 14 mwezi wa Mei kijiji cha Ng’orika kilicho Mbaruk katika kaunti ya Nakuru.
Kulingana na upande wa mashtaka, Kamau alifika nyumbani kwake akiwa mlevi siku ya tukio hilo mwendo wa saa mbili usiku na hapo akamkosa mkewe.
Upande wa mashtaka aidha uliaambia mahakama kuwa mkewe mshtakiwa aliingia nyumbani mwendo wa saa nne usiku na hapo mshtakiwa huyo akaanza kumgombeza huku akimtusi kuwa yeye ni kahaba , tukio ambalo liliwavutia majirani ambao waliwafahamisha maafisa wa polisi waliofika hapo na kumtia mbaroni Kamau.
Mshtakiwa huyo hata hivyo alikubali shtaka hilo na akatozwa na mahakama faini ya shilingi elfu kumi pesa taslimu.
Kesi yake itaendelea tarehe ishirini mwezi huu.