Aliyekuwa mchunguzi mkuu wa serikali Dkt Moses Joel ameiambia mahakama kuwa mwili wa bwenyenye kutoka uingereza Harry Roy Veevers, aliyefariki mwaka 2013 katika eneo la Nyali, ulipatikana na sumu ya kuua wadudu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akitoa ushahidi katika Mahakama ya Mombasa siku ya Jumanne, Joel aliambia mahakama kuwa aligundua sumu aina ya cyhalothrin ambayo hutumika kuua wadudu, tumboni mwa mwendazake.

Aidha, Hakimu Julius Nangea amemtaka mkuu wa sheria Githu Muigai kujulishwa kuhusu kuwepo kwa maafisa wa Interpol kwenye kesi hiyo.

Haya yanajiri baada ya familia ya Veever kutaka maafisa hao kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo.

Richard Veever, ambaye ni mtoto wa mwendazake, aliambia mahakama kuwa babake alitishiwa maisha nchini Uingereza kabla ya kufariki akiwa nchini Kenya.

Mwili wa Harry Roy Veevers ungali unahifadhiwa katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani tangu mwaka 2014, huku familia yake ikizozana kuhusu nchi atakayozikwa.

Roy Veevers yuko na familia mbili, mmoja inayoishi humu nchini huku nyingine ikiishi nchini Uingereza.

Mwili wake ulifukuliwa baada ya kuzikwa kwa takribani mwaka mmoja, kisha kuifadhiwa katika hifadhi ya maiti katika hospitali ya Ukanda wa Pwani.

Roy Veevers alikuwa mmiliki wa mali ya mabiloni ya pesa nchini Uingereza pamoja na eneo la Nyali.