Mwakilishi wa kina mama kaunti ya Nyamira Alice Chae ameitaka serikali ya kitaifa kuendelea kuzipa ripoti familia za wanajeshi waliovamiwa na wanamgambo wa Alshabaab kule El Adde Somalia wiki chache zilizopita. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kule Gesiaga wakati alipotembelea familia ya mwanajeshi mmoja ambaye yungali kujulikana aliko, Chae alisema hatua ya serikali kuzipa familia hizo ripoti kuhusu hali ilivyo kule Somalia itazisaidia pakubwa familia hizo hasa kwa kuwapunguzia mawazo. 

"Yafaa serikali iendelee kuzipa ripoti familia za wajeshi waliotekwa nyara na wanamgambo wa Alshabaab kule El Adde kwa maana familia hizo zina haki ya kujua waliko wapendwa wao," alisema Chae. 

Kwa upande wake babaye mwanajeshi ambaye yungali kujulikana aliko Zachary Osano, serikali haijawai wapa taarifa zozote kuhusu aliko mpendwa wao, huku akiongeza kuwa vyombo vya habari ndivyo vimekuwa vikiwapa ripoti kuhusiana na hali ilivyo kule Somalia.

"Tulizungumza na mwanangu tarehe 14 mwezi Januari na kisha keshoye tukapata taarifa kwamba wanajeshi walikuwa wameshambuliwa kule El Adde Somalia, na tulijaribu kumpigia simu ila ilikuwa ikilia na hakuna mtu alitujibu na tungali tunakumbwa na msongamano wa kimawazo," alisema mzee Osano.