Siku moja tu baada ya bunge la kitaifa kudinda kuidhinisha mswada wa thuluthi tatu ya uwakilishi wa jinsia bungeni, sasa mwakilishi wa kina mama katika kaunti ya Nyamira Alice Chae amejitokeza kulalamikia hali hiyo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu mapema Ijumaa, Chae alishangazwa na sababu iliyowafanya baadhi ya wabunge kukosa kuuidhinisha mswada huo kwa mara ya pili. 

"Kwa kweli ni jambo la kushangaza kwa hali iliyoshuhudiwa bungeni jana baada ya baadhi ya wabunge kudinda kabisa kupigia kura mswada huo ili uidhinishwe na hata kuwaona wengine wakiondoka bungeni ili wasipigie mswada huo kura," alisema Chae. 

Chae aidha aliongeza kwa kuwarahi wabunge kutouona mswada huo kama unaotetea haki za kina mama bali ulio na na nia ya kuhakikisha usawa wa uwakilishi wa jinsia bungeni. 

"Sijui ni sababu ipi inayo wafanya wabunge wa jinsia ya kiume kuona kwamba mswada huu unaowashughulikia kina mama pekee ila ukweli ni kwamba mswada huu ni wakuhakikisha usawa wa jinsia bungeni," aliongezea Chae.