Chama kinachosimamia maktaba nchini kimefadhili shule ya upili ya Nyamoya iliyoko eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii vitabu vya kusoma ambavyo viligharimu shillingi 270,000.

Share news tips with us here at Hivisasa

Shule hiyo ilifadhiliwa vitabu hivyo siku ya Ijumaa katika uwanja wa shule hiyo, kupitia mwanyekiti wa chama hicho Samuel Nyangeso.

Hii ni baada ya wakaazi wa eneo bunge hilo la Bobasi na viongonzi wa eneo hilo kujitolea na kujenga jumba la maktaba katika eneo hilo.

Maktaba hiyo iliyojengwa ni ya pili katika eneo bunge hilo, na njia mojawapo ya kuinua na kuendeleza viwango vya elimu juu katika sehemu hiyo.

“Ili kuinua viwango vya elimu katika eneo letu la Kisii, sharti kila eneo bunge katika kaunti yetu ya Kisii ijenge makataba moja au mbili ili wanafunzi wawe wanapata vitabu vya kusoma na watapita katika mitihani ya kitaifa,” alisema Nyangeso.

“Hakuna haja ya kuwalaumu walimu wanapofeli kufanya vyema katika mtihani, ni ukosefu wa vitabu vya kusoma unasababisha hayo, tukiwa na vitabu vya kusoma katika shule zetu na wanafunzi wakose kupita, hapo walimu lazima wawajibike kujibu maswali,” aliongezea Nyangeso.

Aidha, mkuu huyo aliwashukuru wakaazi na viongonzi waliofanya ujenzi huo wa maktaba katika shule hiyo ya Nyamoya

Mwenyekiti huyo naye alitoa ufadhili wake wa vitabu hivyo vya kusoma vinavyogharimu shillingi 70,000, kando na vile vya chama cha maktaba nchini.