Share news tips with us here at Hivisasa

Chama cha maskauti katika kaunti ya Kisii kimeandaa mkutano ili kuwapa vijana arobaini na tano mafunzo huku kampeni dhidi madawa ya kulevya na pombe ikishika kasi.

Mafunzo hayo ambayo yalianza siku ya alhamisi katika eneo la Etago, Mugirango Kusini, yanatarajiwa kudumu wiki mbili.

Aidha, vijana hao watatakiwa kuwaelimisha wananchi katika wadi tofauti kwenye kaunti dhidi ya madhara ya mihadarati na pombe.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi, mwenyekiti wa chama cha maskauti hao Caleb Ondieki alisema kuwa hii ni mojawapo ya mbinu za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya madawa za kulevya na pombe katika jamii.

“Katika kaunti ya Kisii, tuna wadi 45 na kila wadi inawakilishwa na kijana mmoja ambaye atapokea mafunzo hayo. Baada ya mkutano huu tutaenda kwa kila wadi kuwaeleza wananchi ubaya wa kutumia dawa hizo ili kupunguza idadi ya wanaotumia mihadarati na pombe katika jamii zetu,” alisema Ondieki.

Aliwahimisa watu wanaotumia mihadarati na pombe kuacha kwani zina madhara kwa miili zao.