Waziri wa Afya nchini Dkt Cleopas Mailu ameondoa hofu kuwa chanjo dhidi ya magonjwa ya rubella na ukambi zinaweza kuathiri watoto kama ilivyodaiwa na viongozi wa kanisa.
Kwenye taarifa kwa vyombo ya habari siku ya Alhamisi, Mailu alipinga madai ya viongozi wa kanisa la Katoliki kuwa chanjo hiyo huenda ikasababisha madhara ya afya.
“Sampuli tulizochukua zinathibitisha kuwa chanjo hizo ni salama kwa wananchi hivyo hapafai kuwa na hofu yoyote. Wazazi wanafaa kuhakikisha kuwa wanao wenye umri wa kati ya miezi tisa hada miaka 14 wanapokea chanjo hiyo kabla ya zoezi hilo kukamiliki,” alisema Mailu.
Zoezi la kutoa chanjo dhidi ya magonjwa ya rubella na ukambi litaingia siku yake ya tano hii leo kote nchini.
Hata hivyo, zoezi hilo linakumbwa na changamoto hasa kufuatia hatua ya baadhi ya waumini kususia kuwapeleka wanao kuchanjwa kwa madai kuwa chanjo hiyo ina athari za kiafya.
Chanjo hiyo imeratibiwa kukamilika tarehe 24 mwezi Mei.