Idara ya Afya katika kaunti ya Mombasa imewahimiza wakaazi kutopuuza zoezi la utoaji chanjo ya Ukambi na Pepopunda kwa watoto ili kuhakikisha kuwa wanawakinga na maradhi hayo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurgenzi mkuu wa afya kaunti ya Mombasa Daktari Khajidah Shikely, amesema kuwa zoezi hilo litafanywa katika maeneo ya shule na nyumba hadi nyumba ili kuhakikisha kuwa watoto wote wa umri wa miezi tisa hadi miaka 14 wanapata chanjo hiyo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Daktari Shikely amesema kuwa lengo la zoezi hilo ni kuhakikisha kuwa watoto hawaambukizwi maradhi hayo yaliyo hatari kwa afya ya mtoto huku akiwahimiza wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata chanjo hiyo.

Amewata wazazi kuwa waangalifu na baadhi ya watu wanaopinga chanjo hiyo kwa kueneza kuwa ya kupinga uzazi, akisema kuwa chembechembe za dawa hizo zilifanyiwa ukaguzi wa kina katika mahabari ya serikali na kubaini kuwa chanjo halali.

"Tunawaomba wazazi kutopuuza chanjo ya Ukambi na kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo ili kuzuia kuambukizwa maradhi haya na kuchipuka kwa maradhi mengine ya kiafya," alisema Daktari Shikely.

Zoezi hilo la wiki moja linatarajiwa kuhakikisha kuwa watoto wamepata chanjo hiyo ili kukabiliana na maradhi hayo na kuzuia kuchipuka kwa maradhi mengine sugu ya kiafya.