Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi katika Kaunti ya Uasin Gishu wameombwa kuwalinda wanao wakati huu wa mgomo ili kuwaepusha na visa vya uhalifu au kukosa nidhamu.

Akizungumza afisini mwake siku ya Jumatatu, naibu gavana wa kaunti hiyo Daniel Chemno alisema kuwa wazazi wanapaswa kuwatunza wanao vizuri ili kuwaepusha kujihusisha na unywaji pombe au visa vingine vibaya.

“Wanafunzi wanapaswa kujihusisha na mambo ambayo hayatawaelekeza kutenda maovu au mambo yoyote ya kuharibu maisha yao,” alisema Chemno.

“Wazazi wanapaswa kuhakikisha wanao wanatumia fursa hii kumaliza kazi za shule ambazo walipewa na walimu na pia kuendelea kudurusu,” aliongezea.

Aidha, amewataka wazazi kusaidia kuwafunza wanao kuhusu mambo ya jinsia, na kuongezea kuwa wengi wao hawana ufahamu kuhusu hali ya jinsia, jambo ambalo limesababisha wengi wao kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi usiofaa.

“Wengi wa watoto wetu wameambukizwa magonjwa ya zinaa kwa kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi na wenzao na hata wale waliowazidi umri. Mambo kama hayo yanawasababishia maisha yasiyo na msingi wowote,” aliongezea Chemno.