Chifu Wa Solai Chemasis Samwel Totona anauguza majeraha makali mguuni katika hospitali kuu mjini Nakuru baada ya kufumwa mshale na mpishi mmoja sugu wa pombe haramu kwenye eneo la Arus Majitamu Jumamosi jioni.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akidhibitisha kisa hicho naibu kamishna wa kaunti ndogo ya Rongai David Koskei alisema kuwa, Chifu huyo alikuwa kwenye oparesheni ya kumwaga pombe haramu pale mpishi mmoja kwa jina Kiprono Kiprotich alipanda juu ya mlima na kumfuma chifu huyo mshale.

Koskei alikashifu kitendo hicho akisema kwamba,hii sio mara ya kwanza kwani wapishi wa pombe haramu katika eneo la Legetio walikuwa wamewavamia wazee wa Nyumba Kumi kwa mishale.

"Hiki ni kitendo cha ukiukaji wa sheria na swala hili pia huwa tunashuhudia katika maeneo haya ya Rongai na lazima likomeshwe, kwa hivyo tutawachukulia hatua wahusika wote," Koskei alisema.

Kwa sasa oparesheni Kali ambayo inaongozwa na OCPD Wa Rongai Joseph Mwamburi, DC David Koskei machifu na maafisa wa polisi inaendelea katika eneo hilo la Arus,  kumtafuta Mshukiwa Kiprono Kiprotich ili achukuliwe hatua Kali za kisheria.

Wananchi wametakiwa kutoa habari ambazo zinaweza kusaidia kufanikisha oparesheni hiyo.