Chifu mmoja kutoka eneo la Kiteje, Kaunti ya Kwale, amefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kwa tuhuma za kujaribu kusajili raia wa Somalia kinyume cha sheria.
Chifu wa lokesheni ya Kiteje, Mohamed Saidi Nyaume, anadiwa kujaribu kumsaidia Mohamed Bakari Mbarak, ambaye ana asili ya kisomali, kupata kitambulisho cha kitaifa mnamo Julai 12, 2016 eneo la gatuzo dogo la Matuga.
Chifu Nyaume anadaiwa kushirikiana na Saidi Bakari Mwashambi katika kusaidia kijana huyo kupata kitambulisho hicho.
Raia huyo wa Somalia anadiwa kutumia kitambulisho cha Saidi Bakari Mwashambi, ambaye ni raia wa Kenya, kama baba mzazi.
Watatu hao walifikishwa mbele ya Hakimu Viola Yator.
Mahakama imewaachilia kwa dhamana ya shilingi laki mbili.