Chifu wa Lokesheni ya Biticha, Wadi ya Rigoma Eneo Bunge la Kitutu Masaba Kaunti ya Nyamira Richard Nyanga’au amesema atapambana na majambazi ambao wamekuwa wakisumbua watu katika eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza na Mwandishi huyu wa Habari siku ya Jumanne Jioni, Chifu Nyanga’au alisema majambazi wamekuwa wakiwasumbua wakaazi wa Lokesheni yake hasa katika kijiji cha Sengera na kusema hatalala ila kutafuta mbinu ya kuwakoma majambazi hao ambao wanatekeleza unyama kwa wananchi

Haya yanajiri baada ya siku tano tu tangu majambazi kushambulia familia moja katika kijiji hicho cha Sengera na kumuua msichana mmoja wa umri wa miaka 18.

“Nitashirikiana na Maafisa wa Polisi kuwasaka na kuwatia mbaroni majambazi hawa wanaoendelea kuwaua wakaazi wasio na hatia yoyote,” alihoji Chifu Nyang’au.

Nyang’au alisema kuwa hao majambazi wamezoea kuenda katika eneo hilo na kuwaamsha watu usiku huku wakidai ni Maafisa wa Polisi wa kufanya msako wa pombe bila yeye kuyajua hayo.

Kulingana na Chifu huyo, eneo hilo limekuwa na visa vya ukosefu wa usalama baada ya watu kusumbuliwa huku wakihofia usalama wao.

Kwa sasa huenda wakaazi wa eneo hilo wapate afueni baada ya kuhakikishiwa usalama kufuatiana na maneno yaliyosemwa na Chifu Nyang’au.

Aidha, Chifu Nyang’au amewaomba watu kuukumbatia mradi wa Nyumba Kumi kwa moyo mmoja wanapoenda kuanzisha msako wa kupambana na majambazi hao kujua nani anatekeleza unyama miongoni mwao.

“Kila mtu amjue nani jirani yake maana wakati huu hamna la kubembeleza watu tusiowajua na wanaotisha maisha ya watu,” alisisitiza Chifu Nyang’au.