Machifu watatu kutoka kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini wamepandishwa cheo na kuwa wasaidizi wa naibu kaunti kamishna.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu kamishna katika kaunti ndogo hiyo, Kithinji Ithai alisema machifu hao John Muriuki kutoka kata ndogo ya Mireroni, Peter Kimani kutoka kata ya Rurii na Dominic Kinyanjui wa kata ndogo ya Thayu walipandishwa cheo, na tayari wamepokea barua kutoka kwa tume ya kuwaajiri wafayikazi wa umma.

Akizungumza siku ya Alhamisi ofisini mwake, naibu kamishna huyo aliwashauri maafisa wa utawala kuongeza elimu yao, sio tu katika kupandishwa cheo bali pia waweze kujimudu kimaisha.

Aliongeza kuwa sharti maafisa wa umma wajitolee katika kuwahudumia wananchi, na kuwatahadharisha kuwa watawajibika katika makosa yao wenyewe.

Wakati huo huo, ofisi yake imeweka mikakati ya kuhakikisha usalama umeimarishwa wakati msimu wa Krisimasi unapowadia.

Kithinji alisema kwa mda wa miezi kadhaa iliyopita, visa vya uhalifu vimepungua kwa asilimia kubwa, na wameongeza doria huku wakitambua maeneo kadha wa kadha ambayo maafisa wa usalama wako macho.

Aliwahimiza wananchi kushirikiana na maafisa wa polisi katika kuwapa habari zitakazo saidia kuzima na kuzuia matukio ya uhalifu kutokea.