Chikuzee, msanii kutoka Mombasa, amejitokeza kuzungumzia uhusiano wake na Susumila, anayetamba kwa kibao chake kipya 'Wewe' alichomshirikisha banati kutoka Nairobi Avril.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Uhusiano wa Chikuzee na Susumila ulionekana kuzorota baada ya madai kuibuka kuwa kibao walichokitoa kinamfaidisha Susumila pekee.

Hata hivyo, msanii huyu amesema kuwa hayo ni mambo ambayo hangependa kuyazungumzia kwani japo kuwa yalikuwa yakitukia, kwa sasa yamepitwa na wakati.

Alisema kuwa hana uhasama wowote na msanii yeyote kwa kuwa kutokana na mengi aliyojifunza kwenye tasnia ya muziki anapaswa kuketi na kushughulikia miradi yake anayoifanya kwenye studio.

Chikuzee ambaye aliwika sana miaka ya nyuma kwa ngoma yake 'Sivibaya kujuana' amekuwa akikwepa waandishi wa burudani kwa muda mrefu kwa kusema kuwa hapendi kuzungumzia maswala ambayo yako wazi kabisa.

Alisema wasanii wanaposhirikiana na kutoa nyimbom basi ni lazima nyimbo hiyo iwafaidishe wote kwa kuwa ni akili zao zilizobuni shairi hilo.

“Ifikapo wakati wa kwenda kutumbuiza, inapaswa wasanii wote wahusishwe kikamilifu kwenye hafla hiyo ili mapato yaende kwa wote, kwa kuwa msanii mmoja akifaidika, hilo litaleta ugomvi baina yao,” alisema Chikuzee.

Chikuzee kwa sasa yuko mbioni kuhakikisha anatwaa nafasi yake kwenye ulingo wa muziki Mombasa, baada ya kupata ushindani mkali kutoka kwa wasanii chipukizi wanaoendelea kufanya vyema.