Wanfanyibiashara katika mji wa Kisii wameiomba Serikali ya Kaunti ya Kisii kuwaondoa watoto wa kurandaranda almaarufu Chokoraa katika mji huo baada ya kukosa heshima kwa wafanyibiashara hao.
Wakiongea na Mwandishi wa Habari huyu siku ya Jumatatu katika mji huo, baadhi ya wafanyibiashara hao; Rudiah Kemunto, Damaris Makori, Jerusa Kwamboka walisema Chokoraa hao wamekosa heshima baada ya mmoja wao kumtoa mfanyibiashara mmoja nguo zake Jumapili katika sehemu yao ya kuuzia mboga karibu na jengo la St. Judes lililoko mji wa Kisii.
Serikali ya Kaunti hiyo sasa imekabidhiwa kibarua hicho cha kuwaondoa Chokoraa hao, ambao wameoneka kuongezeka katika mji huo na kutenda vitendo ambavyo havina msingi wowote.
“Tulikuwa tunauza mboga zetu hapa Jumapili jioni ndiposa Chokoraa mmoja akaja bila sisi kumuona na kumtoa mwezetu nguo kwenda juu, tulimpiga kabla atoroka. Wamekuwa kero kwetu kwa muda mrefu sasa na tunaiomba Serikali ya Kaunti yetu kutafuta mbinu ya kuwaondoa Chokoraa hawa katika mji huu,” alihoji Kwamboka.
Wakati uo huo, wafanyibiashara hao waliongezea kuwa, Chokoraa hao mara nyingi wanawaomba pesa na pindi tu mmoja wakiambiwa hamna pesa, wanawatusi na kuanza kuongea maneno machafu na hata kuwaletea aibu mbele ya watu.
“Chokoraa hawa tunapowanyima pesa wanatutusi huku wakitutisha kuwa tutaona. Kwa sasa tunaiomba Serikali yetu ijaribu iwezalo kuwaondoa hapa maana hata tumehofia maisha yetu,” alisema Kemunto akiongeza kuwa baadhi yao hutembea bila nguo, jambo ambalo limetukera na kutushangaza maana hiyo ni kukosa heshima kwa watu wote kwa ujumla.
Aidha, wafanyibiashara hao wamesema kuwa Chokoraa hao huwasumbua wateja wao wanapoenda kununua mboga na hata kuwapelekea baadhi ya wengine kuacha kununua mboga, kitendo ambacho wanasema ni hasara kwao.