Msimamizi mkuu wa Chuo cha ufundi cha Mombasa - TUM Josephat Mwatelah amekana madai kuwa chuo hicho kimepandisha karo ya masomo chuoni inavyodaiwa na wanafunzi.
Mwatelah amesema kuwa hakuna wakati usimamizi wa chuo umewahi kuchukua hatua yoyote bila kuwahusisha viongozi wa wanafunzi, na kutupilia mbali tetesi kuwa chuo hicho kilifanya uamuzi kama huo.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumanne baada ya kufungwa chuo hicho cha TUM, naibu chansela mkuu huyo hata hivyo alikubali kuwa kuna hela zilizoongezwa, hela ambazo zilijumuisha ada ya kufanya ziara za wanafunzi, na kufafanua kuwa walikubaliana na wawakilishi wa wanafunzi.
"Hela za karo hazikuongezwa vile wanafunzi wanadai, na ada ambayo iliweza kuongezwa kwenye malipo ni ile pesa ya kufanya ziara ya wanafunzi na viongozi wa wanafunzi walikuwa na pande zote na kufanya maagano, hayo madai ya karo hayapo na hayana msingi," alisema Mwatellah.
Kwa upande wa viongozi wa wanafunzi ambao waliongea na mwandishi habari huyu walidai kuwa hawakuhusishwa kamwe kwenye suala hilo la kuongezwa karo, na watayataka mamlaka ya chuo hicho kuwajumuisha wanapofanya uamuzi kama huo.
Chuo hicho kilifungwa Jumatatu na wanafunzi wote kutumwa nyumbani baada yao kuzua ghasia na kuanza kuharibu mali huku wakilalamikia kuongezwa kwa karo.