Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kisii, tawi la Keroka, wana kila sababu yakutabasamu, baada ya usimamizi wa chuo hicho kutangaza mipango ya kujenga maktaba ya kisasa.
Akihutubia wanahabari siku ya Ijumaa, mshirikishi wa chuo hicho, Catherine Nyamwanga, alisema kuwa maktaba ambayo iko katika eneo la Otange Plaza, haitoshi kuhifadhi idadi kubwa ya wanafunzi wanaosomea katika chuo hicho.
"Huu ni mpango ambao umechukua muda mrefu kuafikia kwasababu imekuwa vigumu sana kupata ardhi mjini Keroka. Ni habari njema kwetu kwa kuwa tumepata kipande cha ardhi ambapo tutajenga maktaba kubwa itakayo himili idadi kubwa ya wanafunzi," alisema Nyamwange.
Nyamwange aliongeza kuwa ujenzi huo utangoa nanga mapema mwaka ujao baada yakupata mwanakandarasi atakaye jenga maktaba hiyo ya kisasa.
Aliongezea kuwa chuo hicho kina mpango wakutafuta ardhi yakutosha itakayo wawezesha kujenga chuo, ili iwawie rahisi kuhamisha wanafunzi kutoka vyumba vya kukodisha.
"Tunatarajia kuanza kujenga maktaba hiyo mapema mwaka ujao baada yakupata mwanakandarasi atakaye jenga maktaba hiyo. Pia tuna mpango wa kutafuta ardhi tutakapo jenga chuo kama kile cha Kisii, ili wanafunzi wetu wapate mahala pakusomea," alisema Nyamwange.