Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baraza la maimam na wahubiri CIPK, limetoa changamoto kwa serikali kukomesha visa vya mikasa ya moto shuleni, vinavyoendelea kushuhudiwa kila kuchao.

CIPK imeitaka serikali kuingilia kati na kutatua swala hilo ili kunusuru shule zilizosalia kutokana na jinamizi hilo ambalo limeibua hisia kali katika Wizara ya Elimu nchini.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, katibu mkuu wa baraza hilo tawi la Mombasa Sheikh Mohamed Khalifa, alisema suluhu la pekee ni serikali kuweka maafisa wa usalama katika shule zote za bweni.

“Tunataka serikali ipeleke walinda usalama katika shule za bweni haraka iwezekanavyo kuzuia uharibifu unao sababisha hasara,” alisema Sheikh Khalifa.

Kiongozi huyo wa dini amesema hatua ya haraka inafaa kuchukuliwa kwani wazazi ndio wanaoathirika zaidi wanapotakiwa kulipa gharama ya hasara inayotokea.

“Wazazi walikuwa wakilalamika kutokana na karo kuwa juu, sasa wameongezwa mzigo mwingine wa kulipia hasara inayosababishwa na wanafunzi,” alisema Khalifa.

Haya yanajiri baada ya bweni la Shule ya upili ya Malindi, Kaunti ya Kilifi, kuripotiwa kushika moto usiku wa kuamkia Jumatano.

Hapo awali, Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang'i aliambia kamati ya seneti kwamba takribani shule 68 zimeathiriwa na mikasa ya moto mwaka huu pekee, huku akisisitiza kwamba wanafunzi wanaotekeleza uhalifu huo wataadhibiwa.