Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, limesema kuwa halitaunga mkono shinikizo la mrengo wa Cord kutaka kubanduliwa kwa makamishna wa Tume ya IEBC.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Sheikh Mohamed Khalifa, amedai kuwa mwenendo wa mrengo huo hauna nia ya kuifanyia mabadiliko katiba, bali ni njama za kuvurugu usalama wa nchi.
Kwenye mazungumzo na mwanahabari huyu afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumanne, Sheikh Khalifa alisema kuwa iwapo mrengo huo unahitaji kuwabandua maafisa wa Tume ya IEBC, basi njia mwafaka ni kupitia mazungumzo.
Sheikh Khalifa alisema kuwa kama viongozi wa dini watahakikisha kuwa viongozi wa mrengo wa Cord na Jubilee wamekaa pamoja na kuzungumza kwa amani, ili mgogoro unaoendelea kwa sasa nchini kusitishwa kwa kupatikana suluhu la kudumu.
“Sisi kama viongozi wa dini hatujapendezwa na jinsi mrengo wa Cord unavyowachochea wananchi na kusababisha vurugu na ukosefu wa usalama. Iwapo wanataka IEBC ivunjwe, basi njia mwafaka ni kupitia mazungumzo. Tutahakikisha kuwa swala hilo limepata suhulu,” alisema Sheikh Khalifa.
Siku ya Jumatatu ilikuwa mara ya tatu kwa mrengo wa Cord kufanya maandamano wakitaka Tume ya IEBC kuvunjwa.