Katibu Mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, Sheikh Mohammed Khalifa, amepongeza hatua ya Mahakama ICC kutupilia mbali kesi iliyokuwa ikimkabili Naibu Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Sang.
Akiongea na mwandishi huyu afisini wake mjini Mombasa siku ya Jumatano, Sheikh Khalifa alisema kuwa uamuzi huo ulikuwa wa sawa kwani wawili hao hawakuwa na kesi ya kujibu dhidi ya madai hayo.
Sheikh Khalifa amewataka viongozi wa taifa hili kuungana na kufanya maendeleo kwa wananchi huku akishinikiza Wakenya kudumisha amani na kutangamana.
"Tunapongeza uamuzi wa mahakama ya ICC wa kumuachilia huru Naibu Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Sang kwa kupata kesi ile kutokuwa na ushahidi wa kutosha. Kama viongozi wa dini tunawaomba Wakenya kuwa na amani na kutoliingiza swala la uamuzi wa ICC siasa na ukabilia, bali tuwe watulivu na kudumisha amani,” alisema Sheikh Khalifa.
Kiongozi huyo wa dini amewataka Wakenya kujitenga na siasa za kikabila na vyama na kutoliangazia swala la uamuzi wa ICC vibaya kwani hatua hiyo huenda ikachangia vurugu.
Kauli ya Sheikh Khalifa imejiri baada ya majaji wa mahakama ya ICC nchini Uholanzi kutupilia mbali kesi iliyokuwa ikiwakabiliwa Naibu Rais Willium Ruto na mwanahabari Joshua Sang kufuatia ghasia za uchaguzi wa mwaka wa 2007.