Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini CIPK, limetaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kusuluhisha mzozo unaohusiana na shinikizo la kubanduliwa kwa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.
Akizungumza siku ya Jumamosi, katibu mtendaji wa baraza hilo Sheikh Mohammed Khalifa alisema kuwa kama baraza wanapinga vikali maandamano ya Cord ya kushinikiza kubanduliwa kwa makamishna wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.
“Kama baraza tunataka mazungumzo ya haraka kufanyika kati ya serikali na mrengo wa upinzani wa Cord ili kumaliza mzozo unaohusiana na Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC,” alisema Khalifa.
Khalifa aliyataja maandamano hayo kama chanzo cha kutatiza amani na maelewano nchini.